Ubakaji ndani ya ndoa umeongezeka - LHRC
Suala la ubakaji ni kubwa ndani ya ndoa kuliko hata ubakaji wa kawaida. Suala la ubakaji kufanyika ndani ya ndoa kwa wana...
https://mirindimoyapwani.blogspot.com/2014/12/ubakaji-ndani-ya-ndoa-umeongezeka-lhrc.html
Suala la ubakaji ni kubwa ndani ya ndoa kuliko hata ubakaji wa kawaida.
Suala la ubakaji kufanyika ndani ya ndoa
kwa wanando au la, limekuwa linavuta hisia na kupewa mitazamo tofauti
na watu tofauti. Makala hii yazungumzia baadhi watu
wanavyolitazama suala hilo
Rehema Charles John (38) mke na mama wa
watoto na mkazi wa Sombetini, katika Halmashauri ya Jiji la
Arusha, anapata kigugumizi kusema bayana iwapo katika ndoa vitendo vya
ubakaji vipo.
Mwanzoni anakubali kwamba , ubakaji ndani
ya ndoa upo akitoa tafsiri sahihi ya jinsi anavyoelewa ubakaji, kwamba
ni kitendo cha mwanamume kumwingilia mwanamke kimapenzi pasipo mwanamume
huyo kupata ridhaa yake.
Kwa msingi huo, Rehema anajenga hoja
kwamba, hata katika ndoa baadhi ya wanaume wamekuwa wakijikuta
wakitumbukia katika jinai hiyo, pale wanapotumia nguvu na hivyo
kuwalazimisha wake zao kufanya tendo la ndoa.
“ Ninachojua ubakaji ndani ya ndoa
unatokea hasa kwa mwanamume anapotumia nguvu kufanya mapenzi na mkewe,
ambaye kwa wakati huo hajisikii kufanya kitendo kama hicho, anaweza
akawa amechoka au ana matatizo mengine…hivyo, akikataa na mume
kulazimisha hapo ndipo mume anapofanya ubakaji,” anaeleza Rehema ambaye
ni mfanyabiashara katika soko la Kilombero mjini hapa.
Anasema vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa
vinatokea hasa, wakati mume anapokuwa amekunywa pombe hali inayomfanya
kutoelewa cho chote pale anapokataliwa au anapoelewa na mkewe kwamba
hayuko tayari kufanya tendo hilo kwa wakati huo.
“ Hasa mume akiwa amekunywa pombe anakuwa
haangalii na wala hasikii kukuru kakara zinazotokana na yeye
kulazimisha. Mara nyingine mke ambaye hataki kupata aibu mbele ya watoto
wake kutokana na kelele hizo anakubali yaishe ili kulinda heshima,”
anaeleza.
Anasema hakuna mke ambaye anakusudia kumtesa mumewe lakini kama hajisikii kwa siku hiyo atakuwa anabakwa.
“ Ili kuogopa aibu kwa watoto inabidi mke
akubali tu hata kama awali alikataa, inabidi afanye tu na mke anyamaze
ili watoto wasijue baba na mama walikuwa wakifanya mambo hayo usiku,”
anasema.
Hata hivyo, Rehema anaweka wazi kwamba,
mambo kama hayo hayajamtokea yeye kwa kuwa, mumewe ni mtu mstaarabu na
mwenye heshima katika ndoa yao.
Lakini kigugumizi cha Rehema kuhusu
ubakaji ndani ya ndoa kinakuja pale alipoulizwa iwapo anaweza kumshtaki
mumewe kwa kosa la kumbaka.
“ Nitaenda kumshtaki wapi, kwa wazazi
wake au nitaenda kumshtaki mahakamani, ili iweje? Huyo ni mume wangu
itakuwaje nimshtaki,” anahoji na kuongeza, “ kama kuna tatizo ni vema
mwanamke akamweleza mwenzake ili avumilie hadi hapo tatizo
litakapokwisha.”
Kigugumizi kama hicho alikipata pia John
Paulo, baba wa watoto wawili na mkazi wa Moshono mjini hapa. Awali
John, alizungumzia kukubali kwamba ndani ya ndoa kuna ubakaji, lakini
baadaye alisema, hakuna mwanamume anayebaka mke wake.
Msingi wa kukubali kwake awali, ulitokana
na tafsiri aliyoitoa kwamba, kitendo cha ubakaji ni kumwingilia
mwanamke bila ridhaa yake hata kama kitendo hicho, kitakuwa kikifanywa
na mume kwa mkewe.
“ Ubakaji ndani ya ndoa upo pale mmoja
anapofanya kitendo hicho wakati mwingine amechoka au kama hataki kwa
sababu fulani za msingi,” anasema.
Hata hivyo, anasema wapo wake wengine
ambao kutokana na ujeuri wao, wanatumia hiyo kama silaha ya kuwakomoa
waume zao, na hapo ndipo John anapohoji, “sasa mume anapokataliwa na
mkewe aende wapi.”
Anasema katika hali hiyo, inabidi mume
atumie nguvu ili kupata haki yake, lakini anasema likifanyika wakati wa
maelewano linakuwa zuri.
Sheria Maalum ya Makosa ya Kujamiiana ya
mwaka 1998, (SOSPA) inaeleza ubakaji kama kitendo cha mwanamume
kumwingilia mwanamke ukeni, kwa nguvu pasipo ridhaa yake kwa lengo la
kutaka au kufanya naye mapenzi.
Inataja kuwa, kufanya kitendo hicho ni
kosa la jinai ambalo mtuhumiwa akitiwa hatiani anaweza kupata adhabu ya
kifungo cha miaka 30 jela au maisha.
Lakini wakati suala hilo likiwa hivyo,
hivi karibuni, washiriki wa mafunzo yanayotolewa na shirika la Hakikazi
Catalyst la mkoani Arusha kwa wanaharakati, maafisa watendaji wa kata na
vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji wapatao 80 kutoka mikoa ya Tanga,
Kilimanjaro, Arusha na Manyara walizua mjadala mzito wakati mwezeshaji
kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Rehema Mwateba, alipokuwa
akitoa mada yake kuhusu somo la jinsia.
Katika somo hilo, Rehema ambaye ni
mwanaharakati na mchambuzi wa masuala ya kijinsia nchini, alielezea
istilahi zinazohusiana na maumbile, kazi za jinsi, jinsia, malazi,
mahitaji maalum ya kijinsia na mambo kadha wa kadha, pia alizungumzia
suala la kubakwa, kubaka na ubakaji.
Rehema alifafanua kwamba, kubakwa ni
kitendo cha mwanamke kuingiliwa ukeni bila ridhaa yake, wakati kubaka ni
kumwingilia mwanamke wa umri uwao wo wote ule, kwenye uke wake bila
ridhaa yake na ubakaji ni kitendo cha kumwingilia mwanamke ukeni bila
ridhaa yake.
Baada ya tafsiri hizo, ndipo mjadala
ulipozuka kuhusu ubakaji ndani ya ndoa, ambapo vuta ni kuvute ilizuka
kati ya wanaume na wanawake.
Wanaume walikuwa wakisisitiza hakuna
ubakaji ndani ya ndoa, wakati wanawake kwa upande wao walisema wengi wao
wanabakwa na waume zao.
Wanaume waliokuwa wakipinga, walienda
mbali zaidi na kuitaka serikali kuifanyia marekebishao sheria ya SOSPA,
ili tafsiri isemayo ubakaji ni kumwingilia kimwili mwanamke bila ridhaa
yake isiwahusu watu wenye ndoa.
Wakijenga hoja walisema, wakati wa
kufunga ndoa tayari mwanamke anakuwa amekwisharidhia kuwa mke, na kwa
sababu hiyo hakuna haja ya kuridhia mara kwa mara kila wanapohitaji
kufanya tendo hilo.
Mchungaji wa Kanisa la Calvary Assemblies
of God la Tengeru, mkoani Arusha, Vumilia Samuel Isanje, alisema hakuna
ubakaji kwa watu wenye ndoa.
“ Ubakaji kwenye ndoa uondolewe…ni vizuri
mwanamke akaelewa kwamba muda wo wote jambo hilo linaweza kutokea, na
anakuwa amekwisharidhia tangu walipofunga ndoa kufanya tendo hilo na
mumewe, hivyo hakuna haja ya kuridhia mara kwa mara wanapohitaji kufanya
hivyo.
Kwa upande wake, Ezekiel Muhubiri kutoka
asasi ya Kiungo ya mkoani Kilimanjaro, alisema alishauri kuwekewa mipaka
kwa sheria ya SOSPA.
“Sheria hii iwekewe mipaka, hili ni suala
la kuandaana, sheria ifanyiwe marekebisho kwani huko sio kubaka,
bali mwanamke anakuwa hajaandaliwa, lakini kama inakuwa kwa mwanamke wa
nje basi hapo panahitajika ridhaa yake,” alisema.
Lakini wanawake kwa upande wao, walikuwa wakisisitiza kwamba ndani ya maisha ya ndoa ubakaji upo.
Walikuwa wakifafanua kwamba ubakaji
katika ndoa unakuja pale mwanamume anapohitaji kupewa haki yake ya ndoa,
lakini kwa bahati mbaya mwezi wake anakuwa hayupo tayari pengine kwa
sababu za kiafya au kuchoka.
“Ubakaji ndani ya ndoa upo, pale
mwanamke anapokuwa hajisikii kwa tendo hilo lakini mwanamume
analazimisha…hapo anabaka, mwanamke anakuwa hayupo tayari kwa tendo
hilo,” alisema mwanamke mmoja.
Alisema kwa ujumla tendo hilo ni la
maelewano lakini katika mazingira fulani wanaume wanakuwa wakilazimisha
kufanya tendo hilo na hapo ndipo ubakaji unapoingia.
Mshiriki mwingine kutoka kijiji cha
Eworendeke, wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, Nengolong Sadala,
alisema suala la ngono ni la maelewano kati ya mume na mke na
inapotokea mmoja anatatizo fulani mwingine anatakiwa kuwa na uvumilivu.
Akiunga mkono kauli hiyo, mkazi mwingine
wa kijiji hicho, Noorkimunyak Ndoori, alisema anasikia kuwa wapo baadhi
ya wanaume ambao wanalazimisha kwa nguvu kupewa unyumba kwa wake zao
wakati sual hilo ni la maelewano.
“ Unamkuta mwanamke ni mgonjwa au wakati
mwingine amechoka, lakini mwanaume analazimisha apewe haki yake, kufanya
hivyo ni sawa na kubaka,” alisema na kuongeza, “kinachohitajika hapa ni
maelewano na mmoja kumwandaa mwenzake na sio kulazimisha.”


Hata kama awalewi wanabaka tu.
ReplyDelete